Thursday, May 24, 2012
Barua ya watu wa Uzini kwa Rais Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete
Kwa mshangao mkubwa sisi watu wa Uzini tukaletewa mtu alie nje mbali sana na jimbo letu kutoka jimbo la Bububu wilaya ya Magharibi na kuhamishiwa kwenye tawi letu na kupewa fomu ya kugombea nafasi hiyo ya uwakilishi huku wanajimbo halisia wafikao kumi waliojitiokeza kugombea nafasi hii wakiangushwa kwa hila na ghilba na nguvu ya pesa aliyoitumia mwanachama wa CCM mwenzetu, mfanya biashara, bwana Moh’d Raza Daramsy, akisaidiwa na kusimamiwa na viongozi waliokuwa si waaminifu wa chama chetu, ambao wameshindwa kupima upepo wa siasa zetu, na ambao wamesahau historia ya mapinduzi yetu. Viongozi hawa wa ngazi ya jimbo na wilaya wasipoangaliwa kwa umakini mkubwa watakipeleka pabaya chama chetu.
BARUA YA WAZI KWA MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI, CCM TAIFA, AMBAE PIA NI RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE
22/12/2011
Mheshimiwa mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi, kwa heshima kubwa na kwa unyenyekevu uliotukuka juu yako tunaiandika barua hii tukiwa na majonzi makubwa juu ya maafa makubwa yaliyosababishwa na mafuriko yatokanayo na mvua kubwa zilizonyesha katika jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine na kusababisha kupelekea vifo vya watanzania wenzetu na uharibifu mkubwa wa mali na mionombinu. Tunatoa mkono wa pole kwako wewe binafsi kama mkuu wa nchi na kwa familia za wenzetu wote walioathirika na maafa hayo. Tunawaomba watanzania wote tuungane pamoja katika kuwafariji wenzetu hawa kwa hali na mali. Kwa wale ambao roho zao zimepotea, tunamuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi, Amin.
Mhe. Rais, uwamuzi wako wa kukatisha ziara yako mkoani Mara na kurejea Dar es Salaam leo ni uthibitisho kamili kuwa wewe ni kiongozi unaewajali wananchi wako. Tunaamini utatoa kauli ambayo itakuwa ni dira kwa watanzania kuweza kukabiliana na janga hili na majanga mengine ya namna hii ili yasiweze kutokea tena nchini mwetu.
Mheshimiwa, baada ya pole zetu hizo tunaomba kwa umakini sana usikilize kilio chetu sisi wanachama wenzako wa CCM, wa jimbo la Uzini liliyopo wilaya ya Kati, mkoa wa Kusini Unguja. Tunachukua fursa hii muhimu kukuandikia barua yetu hii tukijua wewe ni kiongozi wetu makini, mahiri, msikivu, muajibikaji na mfuatiliaji hata kwa habari ambazo wengine huziona kuwa hazina maana, wewe huzipa umuhimu na kuzifanyia kazi. Hii ndio maana chama chetu cha Mapinduzi CCM, kimekuwa kikipendwa na kuzidi kuungwa mkono, na kimekuwa kikipata ushindi wa kishindo kila uchaguzi mkuu unapofika. Hivyo basi, barua yetu hii ya wazi kwako tunaamini utaichukulia kama ni changamoto na sio ukosefu wa adabu.
Mh. Mwenyekiti hivi sasa muda si mrefu tutaingia katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Uzini kwa nafasi ya uwakilishi ili kujaza nafasi hiyo iliyoachwa wazi na aliyekuwa mwakilishi wetu mpendwa marehemu Maalim Mussa tuliyemchagua kwa kura nyingi za wana CCM. Tunajinasibu na kujilabu kama jimbo hili ni letu tangu asili na dahari na wewe Mheshimiwa hili unalijuwa vizuri kwa sababu wewe ni sehemu yetu na uliishi hapa visiwani na ukakijenga chama cha CCM kilichotokana na Afroshirazi na TANU hapa katika ofisi kuu ya CCM Kisiwandui ukiwa mtendaji.
Mheshimiwa mwenyekiti tulipokea kwa furaha kubwa kalenda ya uchaguzi wa ndani ya chama chetu kwa nia ya kukamilisha taratibu za uchaguzi kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama chetu ili kupata mgombea atakaesimamisha, kuipigania na kuitetea bendera ya chama chetu katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Uzini.
Sisi wazee wa chama na wenyeji wa jimbo hili tukijua huu ni uchaguzi wa jimbo ambao wanajimbo wenyewe wananaoishi ndani ya jimbo ndio wahusika tofauti na uchaguzi wa Rais kwani Rais hana jimbo maalum, ndio maana tukamchagua Dr Ali Moh’d Shein kutoka Pemba kuwa Rais wetu, kwa kuwa Zanzibar ni jimbo moja kwa nafasi ya urais kama tilivyokuchagua wewe kutoka Bagamoyo kuwa rais bwa Jamhuri kwa kuwa Tanzania ni jimbo moja kwa uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya muungano.
Kwa mshangao mkubwa sisi watu wa Uzini tukaletewa mtu alie nje mbali sana na jimbo letu kutoka jimbo la Bububu wilaya ya Magharibi na kuhamishiwa kwenye tawi letu na kupewa fomu ya kugombea nafasi hiyo ya uwakilishi huku wanajimbo halisia wafikao kumi waliojitiokeza kugombea nafasi hii wakiangushwa kwa hila na ghilba na nguvu ya pesa aliyoitumia mwanachama wa CCM mwenzetu, mfanya biashara, bwana Moh’d Raza Daramsy, akisaidiwa na kusimamiwa na viongozi waliokuwa si waaminifu wa chama chetu, ambao wameshindwa kupima upepo wa siasa zetu, na ambao wamesahau historia ya mapinduzi yetu. Viongozi hawa wa ngazi ya jimbo na wilaya wasipoangaliwa kwa umakini mkubwa watakipeleka pabaya chama chetu.
Sisi wazee wa Uzini tunajivunia na kujifagharisha mno na Mapinduzi yetu Matukufu ya mwaka 1964 kwani sisi watu wa Uzini tumetoa mchango mkubwa sana kuyafanikisha Mapinduzi hayo. Kambi za kuandaa Mapinduzi ziliundwa katika jimbo la Uzini. Wapangaji na waratibu wa Mapinduzi wengi wao walitoka katika jiombo la Uzini. Hii ndio maana kati ya wanavuguvugu lililoleta Mapinduzi moja wapo ni Mzee Kesi, mwanasiasa maarufu aliyeshitakiwa na serikali ya kikoloni ya wakati huo ili kumkandamiza Maalim Muhsin. Baadae kwa kuthaminiwa aliteliwa kuwa waziri na MBM katika serikali ya mwanzo baada ya Mapinduzi.
Mwengine ni mzee Muhsin bin Ali ambae nae alipewa uwaziri na Karume kwa kuthamini mchango wake mkubwa na mchango wa watu wa Uzini katika Mapinduzi ya 1964. Na wengi wengineo ambapo ndio maana wazee wetu hawa wa jimbo la Uzini wakatuzalia vijana wazalendo wanamapinduzi kama alivyo Mhe Seif Khatib, Mbunge wa jimbo la Uzini ambae ametoa mchango mkubwa katika kuujenga, kuutetea na kulinda Muungano wa Tanzania. Wengine ni waziri wa elimu wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe Ranadhani Abdalla Shaaban na Mhe Ali Mwinyi Msuko, Afisa mtendaji katika ofisi kuu ya CCM. Na wengine wengi ambao itachukua muda mrefu kuwataja.
Mheshimiwa mwenyekiti, tumeandika haya na kuyafikisha kwako tukitumaini chama chetu bado kina vikao vyake vya juu ambavyo vitafikia maamuzi ya kutuletea mgombea ambae sisi wanachama ndio tutakaokuwa na nafasi kubwa ya kumsimamia ili aweze kushinda. Mhe Mwenyekiti, kwa kutumia vyombo vyako ulivyonavyo ambavyo vina mizizi mirefu vilivyoko ndani ya jimbo tunaamini vitakupa taarifa zilizo sahihi zilizomo ndani ya jimbo hivi sasa baada ya matokeo ya kura ya maoni. Jimbo limegawika na vijiji vimekatika na chama kimetikiswa.
Wako wanaokumbuka kama chama hichi hichi cha CCM kimefanya maamuzi mazito katika chaguzi za nyuma zilizopita kama vile jimbo la Kigamboni pale kilipofuta uteuzi wa Yussuf Manji na pale Kawe kilipofuta uteuzi wa Adam Jee na kwengineko ili kukinusuru chama. Maamuzi kama haya yanahitajika katiaka jimbo la Uzini ili kukinusuru chama hasa kwa jimbo hili la Uzini kwa historia yake, nafasi yake na mchango wake mkubwa kwa chama chetu.
Mheshimiwa mwenyekiti, demokrasia iliyopana ni fujo kwa wale wenye dhamira zao za tamaa na ulwa au kufichia waliyonayo. Kwa mwenendo huu ambao chama chetu kinaendeshwa na baadhi ya watendaji waliokosa uadilifu watatufikisha pahala pabaya jambo ambalo sisi wana CCM wazalendo na wanamapinduzi hatulikubali. Kwani mchelea mwana kulia mwisho hulia yeye. Sauti ya wanyonge ni sauti ya Mungu. Mkoa wa kusini Unguja ni Mkoa ambao hakijatoka kiti chochote kikenda upinzani tokea 1957.
Kwa mwenendo huu sasa ambapo kila mwenye fedha zake nyingi ndie anaefanya maamuzi ya wazalendo ni hatari inayotaka kuepukwa kwa gharama yoyote. Hatuyasemi haya kwa kukusudia ubaguzi sisi ubaguzi hatunao. Lakini jee itakuja kuwa sahihi kama Mkunduchi Haruna Ali Suleiman – Muhindi, kwa Muyuni, Jaku – Muhindi, na kwa Uzini, Raza Daramsy – Muhindi? Tungojee na Chwaka mwakani – Noushad Moh’d. Tuje tumalizie na Koani Abdulsatar Haji Daud. Wote wahindi.
Mheshimiwa mwenyekiti tunakushukuru sana kuchukua muda wako mkubwa sana kwa kusoma barua yetu hii. Tunamalizia kwa kuomba kwako radhi na tunaamini utatusamehe kwani wewe ni kiongozi mwenye busara, na utalifanyia kazi suala nyeti tuliokueleza kwa madhumuni ya kurejesha umoja wetu na kudhibiti ushindi wa jimbo letu.
Wanachama wenzako,
Haji Juma Kibwana wa kijiji cha Uzi,
Omar Haji Mo’hd wa Kijiji cha Umbuji,
Kassim Juma Khatib wa kijiji cha Mgeni haji,
Selemani Bakari Bushiri wa kijiji cha Tunduni,
Fatma Herezi Said wa Kijiji cha Bambi,
Mustafa Khamisi Mustafa wa kijiji cha Kiboje,
Nakla kwa:
1. Makamo mwenyekiti CCM – Zanzibar, Dr Amani Abeid Karume
2. Naibu Katibu Mkuu CCM – Zanzibar, Vuai Ali Vuai
3. Wahariri wa vyombo vyote vya habari Tanzania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment