No Pain No Gain Maishani

Saturday, December 11, 2010

Msamaha wa Rais wawapita kando mafisadi, ‘mafataki’


Exuper Kachenje
RAIS Jakaya Kikwete amewatosa mafisadi na waliowakatisha masomo wanafunzi kwa kuwapa mimba kwenye msamaha alioutoa jana kwa wafungwa 3,563 kusherekea miaka 49 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Taarifa iliyotolewa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha imeeleza msamaha wa wafungwa 3,563 uliotolewa na Rasi Jakaya Kikwete wakati wa sherehe za Uhuru mwaka huu hawahusu wafungwa wa makosa ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka, hawahusiki na msamaha huo.

Taarifa hiyo imetaja wafungwa wengine wasiohusika na msamaha huo kuwa ni wafungwa waliowapa mimba wanafunzi na kuwakatisha masomo, waliohukumiwa kunyongwa na waliojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Wengine ni wale waliohukumiwa kifungo cha maisha, waliofungwa kwa makosa ya ujambazi, wizi wa magari na waliofungwa kwa kunajisi, kubaka na kulawiti.

Msamaha huo pia hauwahusu watu wanaotumikia kifungo cha pili au zaidi, wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi za Parole ya mwaka 1994 na Sheria ya huduma kwa jamii ya mwaka 2002.

"Wafungwa wengine ambao hawamo kwenye msamaha huo ni waliozuia watoto kupata masomo, waliowahi kutoroka chini ya ulinzi, waliohukumiwa kwa makosa ya uharibifu wa miundombinu kama wizi wa nyaya za simu, umeme, njia za reli na transfoma na wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo kwa msamaha wa Rais na bado wanaendelea na kifungo kilichobaki," imeeleza taarifa hiyo.

Rais Kikwete ametoa msamaha huo akitumia Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayompa mamlaka kusamehe wafungwa siku za sherehe za Kitaifa ambazo ni Uhuru na Muungano.

Tanzania Bara ilipata Uhuru wake kutoka kwa Mwingereza Desemba9, 1961.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya waziri Nahodha, wafungwa wanaonufaika na msamaha huo ni wale wanaotumikia kifungo kisichozidi miaka mitano na ambao hadi jana walishatumia robo ya vifungo vyao na wafungwa ambao ni wagonjwa wa Ukimwi, kifua kikuu, saratani ambao wanaoelekea siku za mwisho wa maisha yao na wazee wa zaidi wenye umri wa zaidi ya miaka 70.

Hata hivyo wafungwa hao watatakiwa kuthibitishwa na jopo la madaktari chini ya mganga mkuu wa mkoa au wilaya.

Taarifa hiyo imetaja wafungwa watakaonufaika na msamaha huo kuwa ni wanawake waliofungwa wakiwa wajawazito, walioingia magerezani wakiwa na watoto wachanga wanaonyonya na wenye ulemavu wa mwili na akili ambao ulemavu wao utathibitishwa na mganga mkuu wa mkoa au wilaya.

“Ni mategemeo yetu kwamba watakaoachiwa huru watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee gerezani,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya serikali.

No comments:

Post a Comment