Thursday, October 28, 2010
Hatimaye JK azindua mradi wa mabasi kasi
Ummy Muya
HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete jana alizindua awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo kasi, akisema kuwa tatizo sugu la msongamano wa magari jijini Dar es salaam litapungua baada ya kukamilika kwa awamu hiyo.
Rais alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akiweka jiwe la msingi kama ishara ya kuzindua ujenzi wa miundombinu ya mradi huo ambayo itahusisha barabara ya mabasi yanayotoka eneo la Feri kuanzia Kivukoni hadi Kimara.
Alisema wakati Wizara ya Miundombinu ikiwa katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi atakayejenga barabara hiyo yenye jumla kilomita 20.9 kwa awamu ya kwanza, ujenzi kwa awamu zote sita unatarajiwa kukamilika mwaka 2025.
Mradi huo mkubwa uliotangazwa kwa mara ya kwanza mwaka 2003 unajengwa kutokana na mkopo wa takriban Sh185 bilioni kutoka Benki ya Dunia, huku serikali ikitakiwa kuchangia fedha za kulipa fidia kwa watakaoathiriwa na mradi huo.
"Ili kupunguza msongamano huo, maeneo ya Ubungo Mataa na Tazara ndio yatakuwa ya kwanza kujengwa barabara za juu na kufuatiwa na Magomeni, Fire, Kamata na Chang'ombe," alisema Rais Kikwete.
"Serikali inaangalia uwezekano wa kutumia treni kwa ajili ya kutoa huduma za usafiri wa katikati ya mji kwa njia ya Ubungo, Buguruni, Mabibo, Tabata na baadaye Kimara hadi Tegeta."
Tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es salaam linazidi kuwa kubwa kadri siku zinavyokwenda kutokana na ongezeko la magari na idadi ya watu ambao sasa ni zaidi ya milioni 4.
Mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia, John Mclntire alisema katika hafla hiyo kuwa jiji la Dar es Salaam linapata wakazi wapya takribani hamsini kila siku jambo linalofanya msongamato na shida ya usafiri wa haraka kupatikana.
Mclntire alisema elimu na ushirikianao vinahitajika kutokana na mradi wa ujenzi huo kufanyika nyakati za asubuhi na mchana wakati wananchi wengine wakizitumia barabara hizo.
Alisema shughuli hiyo ifanyike kwa ufanisi na mafanikio kunahitajika ushirikiano baina ya kitengo cha usalama barabarani, Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra), Wizara ya Miundombinu na Wakala wa Barabara (Tanroads).
"Hadi fikapo mwaka 2020 Dar es salaam itakuwa na wakazi mara mbili na waliopo sasa hivyo ni budi kuanza kuimarisha miundombinu ili kusiwepo na msongamano," alisema.
Naye Waziri wa Miundombinu, Dk Shukuru Kawambwa alisema ujenzi huo utakuwa na awamu sita na katika awamu ya kwanza mradi huo wenye kilomita 20.9 kutoka Kivukoni hadi Kimara.
Dk Kawambwa alisema awamu hiyo ya kwanza ya mradi huo utahusisha ujenzi wa vituo vikubwa vitano, vidogo sita, karakana mbili za mabasi na kuhamisha miundombinu ya umeme.
"Mikataba iliyokamilika ni ile ya kujenga karakana, kuhamisha miundombinu ya umeme na vituo vya mabasi na makampuni yaliyopata kazi hizi ni Beijing Constructions Engineering ya China itakayojenga karakana na vituo vya mabasi na Spencon Service Ltd ya Tanzania itakayohamisha miundombinu ya umeme," alisema.
Alisema awamu ya pili ya mradi huo itahusu Barabara ya Kilwa yenye urefu wa kilomita 19.3, awamu ya tatu itahusisha Barabara ya Nyerere yenye urefu wa kilomita 23.6,awamu ya nne barabara ya Ali Hassan Mwinyi yenye urefu wa kilomita 16.1 awamu ya tano Barabara ya Mandela yenye urefu wa kilomita 22.8 na awamu ya sita itahusu Barabara ya Shekilango na Old Bagamoyo zenye jumla ya kilomita 27.6
Dk Kawabwa alisema kuwa barabara hizo zitakuwa na upana wa mita 6.6 na zitajengwa katikati ya barabara zilizopo sasa na zitakuwa na njia moja kwa kila uelekeo, na katika vituo vya kushusha na kupakia abiria kutakuwa na njia mbili kwa kila uelekeo ili kuweza kupishana kwa haraka
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment